KESI INAYOMKABILI TIDO MHANDO KUSIKILIZA MACHI 28
Kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando ya matumizi mabaya ya madaraka inatarajiwa kuanza kusikilizwa Machi 28, mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja baada ya Tido kusomewa maelezo ya awali (PH) leo Februari 28,
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victoria Nongwa.
Kabla ya kusomewa PH, Tido alikumbushwa mashtaka yake yanayomkabili na Wakili wa Serikali Dismas Mganyizi.
Katika maelezo hayo ya awali, Tido amekubali maelezo yake binafsi ya kwamba alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC mwaka 2006 hadi 2010 na kuwa alikuwa msimamizi katika shughuli za TBC lakini siyo kwa shughuli zote.
Pia alikubali kutoa maelezo katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) lakini hakukiri na kuwa alifikishwa mahakamani Januari 26,2018.
Aidha, Tido alikana mashtaka yote yanayomkabili na kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa upande wa mashtaka kuleta mashahidi wao Machi 28,2018.
Mhando anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Inadaiwa kuwa Juni 16, 2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.
Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Mhando aliisababishia TBCli hasara ya Sh887,122,219.19.
Post a Comment